1. Kwa vile sheria ni kivuli tu cha mambo mema yatakayokuja na si picha kamili ya mambo yale halisi, tambiko zilezile za sheria zinazotolewa mwaka hata mwaka, haziwezi kamwe kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu!
2. Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na tambiko hizo zote zingekoma.
3. Lakini tambiko hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao.
4. Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi.
5. Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu:“Hukutaka tambiko wala sadaka,lakini umenitayarishia mwili.
6. Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi.
7. Hapo nikasema:‘Niko hapa, ee Mungu, kutimiza matakwa yakokama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha sheria.’”
8. Kwanza alisema: “Hutaki wala hupendezwi na tambiko, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi.” Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na sheria.
9. Kisha akasema: “Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya matakwa yako.” Hivyo Mungu alibatilisha tambiko za zamani na mahali pake akaweka tambiko nyingine moja.
10. Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza matakwa ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile tambiko ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha.