10. yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji. Mtu huyo atateseka ndani ya moto wa madini ya kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwanakondoo.
11. Moshi wa moto unaowatesa hupanda juu milele na milele. Watu hao waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa alama ya jina lake, hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana.”
12. Hivyo, ni lazima watu wa Mungu, yaani wale wanaotii amri za Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu.
13. Kisha, nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika! Heri watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na Bwana.” Naye Roho asema, “Naam! Watapumzika kutoka taabu zao; maana matunda ya jasho lao yatawafuata.”
14. Kisha, nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya wingu hilo alikuwako aliye kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu kichwani, na kushika mundu mkali mkononi mwake.
15. Kisha malaika mwingine akatoka hekaluni, na kwa sauti kubwa akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, “Tafadhali, tumia mundu wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia yameiva.”
16. Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa.
17. Kisha, malaika mwingine akatoka katika hekalu mbinguni akiwa na mundu wenye makali.
18. Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka madhabahuni, akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali, “Nawe tia huo mundu wako mkali, ukakate vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva!”
19. Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu, chombo cha ghadhabu ya Mungu.
20. Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje ya mji, na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko wenye kina kufikia hatamu za farasi na urefu upatao kilomita 300.