12. Hapo Yosefu akawaondoa wanawe kwenye magoti ya baba yake, kisha akainama kwa heshima.
13. Yosefu akawainua wanawe wawili, Efraimu katika mkono wake wa kulia, akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa baba yake, na Manase katika mkono wake wa kushoto, akimwelekeza kwenye mkono wa kulia wa baba yake, akawasogeza kwa babu yao.
14. Lakini Israeli akaipishanisha mikono yake: Mkono wake wa kulia akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, aliyekuwa mzaliwa wa kwanza.
15. Kisha Israeli akambariki Yosefu, akisema,“Mungu ambaye babu zanguAbrahamu na Isaka walimtii maishani mwao,Mungu ambaye ameniongoza maishani mwangu hadi leo,
16. na malaika ambaye aliniokoa katika mabaya yote,na awabariki vijana hawa!Jina langu na majina ya wazee wangu, Abrahamu na Isaka,yadumishwe katika vijana hawa;nao waongezeke kwa wingi duniani.”
17. Yosefu alipoona kwamba baba yake ameuweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa cha Efraimu hakupendezwa. Basi, akaushika mkono wa baba yake, akitaka kuuondoa juu ya kichwa cha Efraimu auweke juu ya kichwa cha Manase.
18. Akamwambia baba yake, “Sivyo, baba! Huyu hapa ndiye mzaliwa wa kwanza. Tafadhali, uweke mkono wako wa kulia juu ya kichwa chake.”
19. Lakini baba yake akakataa, akisema, “Najua, mwanangu, najua. Wana wa Manase pia watakuwa taifa kubwa na mashuhuri. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, na wazawa wake watakuwa mataifa mengi.”