53. Kisha akatoa vito vya fedha na dhahabu na nguo, akampa Rebeka. Pia aliwapa ndugu na mama yake Rebeka mapambo ya thamani kubwa.
54. Mtumishi wa Abrahamu na watu aliokuja nao wakala, wakanywa na kulala huko. Walipoamka asubuhi, mtumishi yule akasema, “Naomba kurudi kwa bwana wangu.”
55. Lakini ndugu na mama yake Rebeka wakasema, “Mwache msichana akae nasi muda mfupi, kama siku kumi hivi; kisha anaweza kwenda.”
56. Lakini yeye akasema, “Tafadhali, msinicheleweshe, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekwisha fanikisha safari yangu; naomba mniruhusu kurudi kwa bwana wangu.”
57. Nao wakasema, “Basi, tumwite msichana mwenyewe, tumwulize.”
58. Wakamwita Rebeka na kumwuliza, “Je, utakwenda na mtu huyu?” Naye akajibu, “Nitakwenda.”
59. Basi, wakamwacha Rebeka na yaya wake aende na mtumishi wa Abrahamu na watu wake. Yaya wake Rebeka pia aliandamana naye.
60. Basi, wakambariki Rebeka wakisema,“Ewe dada yetu!Uwe mama wa maelfu kwa maelfu;wazawa wako waimiliki miji ya adui zao.”
61. Kisha, Rebeka na wajakazi wake wakapanda ngamia na kumfuata huyo mtumishi wa Abrahamu; nao wote wakaondoka.
62. Wakati huo, Isaka alikuwa ameondoka Beer-lahai-roi, akawa anakaa huko pande za Negebu.
63. Siku moja jioni, Isaka alikwenda mashambani kutafakari. Basi, akatazama akaona ngamia wanakuja.
64. Naye Rebeka alipotazama na kumwona Isaka, alishuka chini
65. na kumwuliza mtumishi wa Abrahamu, “Ni nani yule mtu anayetembea kule shambani, anakuja kutulaki?” Yule mtumishi akasema, “Ni bwana wangu.” Basi, Rebeka akatwaa shela yake, akajifunika uso.
66. Yule mtumishi akamsimulia Isaka yote aliyokuwa ameyafanya.
67. Basi, Isaka akamchukua Rebeka ndani ya hema iliyokuwa ya Sara mama yake, akawa mke wake. Isaka akampenda Rebeka na kupata faraja baada ya kifo cha mama yake.