4. Lakini kabla ya kulala usiku, wanaume wote wa mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, bila kubaki hata mmoja, wakaizingira nyumba ya Loti.
5. Wakamwita Loti na kumwuliza, “Wako wapi wale wanaume waliokuja kwako? Watoe nje. Tunataka kulala nao.”
6. Loti akatoka nje, akafunga mlango nyuma yake,
7. akawaambia, “Ndugu zangu, nawasihi msitende uovu huo.
8. Tazama, ninao binti wawili ambao bado hawajalala na mwanamume. Mniruhusu niwapeni hao wasichana muwatendee kama mpendavyo. Lakini msiwatende lolote wanaume hawa kwa sababu ni wageni wangu.”
9. Lakini wao wakasema, “Tupishe! Wewe ulikuja huku ukiwa mgeni na sasa wajifanya hakimu! Basi, tutakutenda mabaya zaidi ya hao wageni wako.” Hapo wakamsukuma Loti nyuma hata karibu wauvunje mlango wake.
10. Lakini wale wageni wakanyosha mikono yao, wakamvuta Loti ndani ya nyumba na kuufunga mlango.
11. Kisha wakawapiga kwa kuwapofusha macho wanaume wote waliokuwapo mlangoni, wakubwa kwa wadogo, hata wakataabika kuutafuta ule mlango, wasiupate.
12. Wale watu wawili wakamwambia Loti, “Je, una mtu mwingine hapa, pengine wana, mabinti, wachumba wa binti zako au watu wengine wa jamaa yako wanaoishi mjini humu? Watoe mahali hapa haraka,
13. kwa maana kilio kilichomfikia Mwenyezi-Mungu dhidi ya wakazi wa hapa ni kikubwa mno, naye ametutuma tuje kuwaangamiza.”
14. Basi, Loti akawaendea wachumba wa binti zake, akawaambia, “Haraka! Tokeni mahali hapa, maana Mwenyezi-Mungu atauangamiza mji huu.” Lakini wao wakamwona kama mtu mcheshi tu.
15. Kulipokucha, malaika wakamhimiza Loti wakisema, “Amka, mchukue mkeo na hawa binti zako wawili msije mkaangamia wakati mji huu unapoadhibiwa.”
16. Loti akawa anasitasita. Lakini kwa vile Mwenyezi-Mungu alivyomhurumia Loti, wale malaika wakamshika yeye, mkewe na binti zake wawili, wakamtoa nje ya mji.
17. Walipowatoa nje ya mji, malaika mmoja wao akawaambia, “Kimbieni kwa usalama wenu. Msiangalie nyuma wala kusimama popote bondeni. Kimbilieni milimani, msije mkaangamia.”
18. Loti akawaambia, “La, bwana zangu!
19. Ni kweli kwamba mimi mtumishi wenu nimepata fadhili mbele yenu, nanyi mmenionea huruma sana kwa kuyaokoa maisha yangu; lakini milimani ni mbali mno. Maangamizi haya yatanikuta kabla sijafika huko, nami nitakufa.
20. Tazameni, kule kuna mji mdogo ambao naweza kuukimbilia kwani uko karibu. Basi, mniruhusu nikimbilie huko. Ule ni mji mdogo tu, na huko nitasalimika.”
21. Naye akamjibu, “Sawa, nimekubali ombi lako. Sitauangamiza mji ulioutaja.
22. Harakisha! Kimbilia huko, nami sitafanya lolote mpaka utakapowasili huko.” Hivyo mji huo ukaitwa Soari.