10. Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, “Sikilizeni, mkaelewe!
11. Kitu kinachomtia mtu unajisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu unajisi.”
12. Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?”
13. Lakini yeye akawajibu, “Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakupanda, utangolewa.
14. Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni.”
15. Petro akasema, “Tufafanulie huo mfano.”
16. Yesu akasema, “Hata nyinyi hamwelewi?
17. Je, hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutolewa nje chooni?
18. Lakini mambo yatokayo kinywani hutoka moyoni, na hayo ndiyo yanayomtia mtu unajisi.
19. Maana moyoni hutoka mawazo ya uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na kashfa.
20. Hayo ndiyo yanayomtia mtu unajisi. Lakini kula chakula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”
21. Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni.
22. Basi, mama mmoja Mkanaani wa nchi hiyo alimjia, akapaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo.”
23. Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele.”
24. Yesu akajibu, “Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo.”
25. Hapo huyo mama akaja, akamsujudia, akasema, “Bwana, nisaidie.”
26. Yesu akamjibu, “Si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
27. Huyo mama akajibu, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao.”
28. Hapo Yesu akamjibu, “Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka.” Yule binti yake akapona wakati huohuo.