Mathayo 13:38-52 Biblia Habari Njema (BHN)

38. Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale ambao ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu.

39. Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho wa nyakati na wavunaji ni malaika.

40. Kama vile magugu yanavyokusanywa na kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati;

41. Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu,

42. na kuwatupa katika tanuri ya moto, na huko watalia na kusaga meno.

43. Kisha, wale wema watangara kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie!

44. “Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile.

45. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri.

46. Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda, akauza yote aliyokuwa nayo, akainunua lulu ile.

47. “Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina.

48. Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa.

49. Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: Malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema,

50. na kuwatupa hao wabaya katika tanuri ya moto. Huko watalia na kusaga meno.”

51. Yesu akawauliza, “Je, mmeelewa mambo haya yote?” Wakamjibu, “Naam.”

52. Naye akawaambia, “Hivyo basi, kila mwalimu wa sheria anayekuwa mwanafunzi wa ufalme wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.”

Mathayo 13