62. Yesu akajibu, “Naam, mimi ndiye. Tena, mtamwona Mwana wa Mtu amekaa upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija katika mawingu ya mbinguni.”
63. Hapo kuhani mkuu akararua joho lake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi?
64. Mmesikia kufuru yake! Nyinyi mwaonaje?” Wote wakaamua kwamba anastahili kuuawa.
65. Basi, baadhi yao wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, wakampiga na kumwambia, “Bashiri ni nani amekupiga!” Hata watumishi wakamchukua, wakampiga makofi.
66. Petro alipokuwa bado chini uani, mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu alikuja.
67. Alipomwona Petro akiota moto, alimtazama, akamwambia, “Hata wewe ulikuwa pamoja na Yesu Mnazareti.”
68. Lakini Petro akakana, “Sijui, wala sielewi unayosema!” Kisha Petro akaondoka, akaenda nje uani. Hapo jogoo akawika.