Kumbukumbu La Sheria 3:11-17 Biblia Habari Njema (BHN)

11. (Mfalme Ogu ndiye peke yake aliyesalia miongoni mwa Warefai. Kitanda chake kilichotengenezwa kwa chuma, kilikuwa na urefu wa mita nne na upana wa karibu mita mbili, kadiri ya vipimo vya kawaida. Kitanda hicho bado kipo katika mji wa Waamori wa Raba.)

12. “Tulipoitwaa nchi hiyo, niliwapa makabila ya Reubeni na Gadi eneo la kuanzia kaskazini mwa Aroeri karibu na Arnoni na nusu ya eneo la milima ya Gileadi, pamoja na miji yake.

13. Kisha nililipatia nusu ya lile kabila la Manase sehemu iliyobaki ya Gileadi pamoja na Bashani yote iliyotawaliwa na Ogu, yaani eneo lote la Argobu. (Nchi yote ya Bashani ilijulikana kama nchi ya Warefai.)

14. Yairi, mtu wa kabila la Manase, alichukua eneo lote la nchi ya Argobu, yaani Bashani, hadi kwenye mpaka wa Geshuri na Maaka. Vijiji vyote alivipa jina lake, na hadi leo vinajulikana kama vijiji Hawoth-yairi.

15. Watu wa ukoo wa Makiri wa kabila la Manase niliwapa Gileadi,

16. na watu wa makabila ya Reubeni na Gadi niliwapa nchi yote kutoka Gileadi hadi mto Arnoni. Mpaka wao wa kusini ulikuwa katikati ya mto na wa kaskazini ulikuwa mto Yaboki ambao ndio unaopakana na nchi ya Waamori.

17. Upande wa magharibi nchi yao ilienea hadi mto Yordani, toka ziwa Galilaya upande wa kaskazini, ukashuka hadi bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, mpaka miteremko ya Pisga, upande wa mashariki.

Kumbukumbu La Sheria 3