Isaya 27:9-13 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Hivi ndivyo uovu wa wazawa wa Yakobo utakavyoondolewa,hivi ndivyo dhambi yake itakavyofutwa kabisa:Ataziharibu madhabahu za miungu;mawe yake yatasagwasagwa kama chokaa;Ashera, wala madhabahu za kufukizia ubani hazitabaki.

10. Mji ule wa ngome sasa umekuwa mtupu,umeachwa na kuhamwa kama jangwa,humo ndama wanalisha na kupumzika.

11. Matawi ya miti yamekauka na kuvunjika;kina mama huyaokota wakawashia moto.Watu hawa hawajaelewa kitu,kwa hiyo Mungu, Muumba wao, hatawahurumia,yeye aliyewafanya, hatawafadhili.

12. Siku hiyo, kutoka mto Eufrate hadi mpakani mwa Misri, Mwenyezi-Mungu ataipura nafaka yake, nanyi Waisraeli mtakusanywa mmojammoja.

13. Siku hiyo, tarumbeta kubwa itapigwa na watu wote wa Israeli waliopotea nchini Ashuru au waliotawanywa nchini Misri watarudi na kumwabudu Mwenyezi-Mungu juu ya mlima mtakatifu huko Yerusalemu.

Isaya 27