Hesabu 18:11-22 Biblia Habari Njema (BHN)

11. “Pia, vitu vingine vyote watakavyonitolea Waisraeli kama sadaka za kutikisa, vitakuwa vyako. Ninakupa wewe, wanao na binti zako kuwa haki yenu milele. Mtu yeyote katika jamaa yako asiye najisi anaweza kula vitu hivyo.

12. “Ninakupa vitu vyote vizuri vinavyotokana na malimbuko ambayo Waisraeli hunitolea: Mafuta safi, divai na nafaka.

13. Mazao yote ya kwanza ya matunda mabivu ya mashamba yao ambayo wataniletea mimi, yatakuwa yako. Kila mtu asiye najisi katika jamaa yako anaweza kula.

14. Kila kitu kilichowekwa wakfu nchini Israeli kitakuwa chenu.

15. “Kila mzaliwa wa kwanza ambaye Waisraeli watanitolea, akiwa mzaliwa wa kwanza wa binadamu, au wa mnyama, atakuwa wako. Walakini huna budi kuwakomboa wazaliwa wa kwanza wote wa binadamu, na kila mzaliwa wa kwanza wa mnyama aliye najisi ni lazima akombolewe.

16. Wazaliwa hao wa kwanza watakombolewa wakiwa wenye umri wa mwezi mmoja kwa kulipiwa fedha shekeli tano, kulingana na vipimo vya hema takatifu.

17. Lakini wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe, kondoo au mbuzi wasikombolewe; hao ni watakatifu. Damu yao utainyunyizia madhabahu na mafuta yao utayateketeza kuwa sadaka ya kuteketezwa ambayo ni harufu nzuri inipendezayo mimi Mwenyezi-Mungu.

18. Nyama yao unaweza kuila, kama vile kidari na mguu wa nyuma wa kulia vinavyotolewa kama sadaka ya kutikisa.

19. “Ninakupa wewe, wanao na binti zako, vitu vyote ambavyo watu wa Israeli hunitolea; hivyo ni haki yenu daima. Hili ni agano la milele mbele yangu ambalo ni kwa ajili yako na wazawa wako.”

20. Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Wewe hutakuwa na urithi wowote katika nchi yao, wala kuwa na fungu lako miongoni mwao; mimi ndimi fungu lako na urithi wako kati ya Waisraeli.”

21. “Kuhusu Walawi, hao nimewapa zaka zote ambazo Waisraeli hunitolea kuwa urithi wao. Haya yatakuwa malipo yao kwa huduma wanayotoa katika kulitunza hema langu la mkutano.

22. Na tangu sasa, watu wengine wa Israeli wasilikaribie hema la mkutano wasije wakatenda dhambi na kujiletea kifo.

Hesabu 18