20. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni,
21. “Jitengeni na watu hawa, niwaangamize sasa hivi.”
22. Lakini Mose na Aroni wakajitupa chini kifudifudi na kusema, “Ee Mwenyezi-Mungu uliye asili ya uhai wa binadamu wote. Je, mtu mmoja akikukosea, utaikasirikia jumuiya nzima?”
23. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,
24. “Waambie watu waondoke karibu na makao ya hema ya Kora, Dathani na Abiramu.”
25. Basi, Mose akaenda kwa Dathani na Abiramu, akifuatwa na wazee wa Israeli.
26. Alipofika, akawaambia watu, “Tafadhalini ondokeni kwenye hema za watu hawa waovu na msiguse kitu chao chochote, msije mkaangamizwa pamoja nao kwa sababu ya dhambi zao zote.”
27. Watu wakaondoka kwenye makao ya Kora, Dathani na Abiramu.Dathani na Abiramu wakatoka mahemani mwao na kusimama mlangoni wakiandamana na wake zao na watoto wao wote hata wale wanaonyonya.
28. Hapo Mose akawaambia watu, “Hivi ndivyo mtakavyotambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyenituma kufanya mambo haya yote, wala siyo kwa matakwa yangu mwenyewe.
29. Watu hawa wakifa kifo cha kawaida, au wakipatwa na maafa kama watu wengine, basi jueni kuwa Mwenyezi-Mungu hakunituma.
30. Lakini Mwenyezi-Mungu akifanya jambo ambalo halijapata kutendeka, ardhi ikafunuka na kuwameza watu hawa pamoja na kila kitu chao, wakaenda kuzimu wakiwa hai, basi mtajua kuwa watu hawa wamemdharau Mwenyezi-Mungu.”