4. basi, yule atoaye sadaka yake, atamletea pia Mwenyezi-Mungu sadaka ya nafaka ya kilo moja ya unga laini uliokandwa na kuchanganywa na lita moja ya mafuta;
5. pamoja na divai ya sadaka ya kinywaji, lita moja, vitu hivyo vitaandamana na kila mnyama wa tambiko ya kuteketezwa: Kondoo au mbuzi.
6. Wakati wa kutoa sadaka ya kondoo dume, kilo mbili za unga uliokandwa na lita moja u nusu ya mafuta vitatolewa kama sadaka ya nafaka,
7. pamoja na sadaka ya kinywaji ya lita moja u nusu ya divai, na kufanya harufu nzuri ya sadaka haya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.
8. Wakati mtakapomtolea Mwenyezi-Mungu fahali kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa au tambiko ili kutimiza nadhiri au kwa ajili ya sadaka za amani,
9. mtu atamtoa kama sadaka pamoja na sadaka ya nafaka ya unga wa kilo tatu ulio mzuri na lita 2 za mafuta,
10. pamoja na sadaka ya kinywaji ya lita 2 za divai, na kufanya harufu nzuri ya sadaka ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.
11. “Hivyo ndivyo vitu vitakavyotolewa pamoja na kila fahali, kondoo dume au mbuzi.
12. Hesabu ya vitu hivyo itaongezwa kulingana na hesabu ya wanyama watakaotolewa.
13. Kila mwananchi Mwisraeli atafuata maagizo hayo wakati anapotoa tambiko, harufu impendezayo Mwenyezi-Mungu.
14. Na kama kuna mgeni anayeishi pamoja nanyi kwa muda au daima, akitaka kutoa sadaka yake kwa kuiteketeza, harufu impendezayo Mwenyezi-Mungu, mtu huyo atafanya kama mnavyofanya nyinyi.
15. Katika vizazi vyote vijavyo, kanuni zilezile mtakazofuata nyinyi ndizo atakazofuata mgeni yeyote atakayeishi pamoja nanyi; mbele ya Mwenyezi-Mungu mtakuwa sawa;
16. nyinyi na yeye mtakuwa chini ya sheria ileile moja na maagizo yaleyale.”
17. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waeleze
18. Waisraeli kwamba wakati watakapoingia katika nchi ninayowapeleka
19. kila mtakapokula mazao ya nchi hiyo, mtatenga kiasi fulani na kunipa mimi Mwenyezi-Mungu.