Hesabu 11:17-27 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Nitashuka huko na kuzungumza nawe; nitachukua sehemu ya roho niliyokupa, niwape watu hao. Nao watabeba jukumu la kuwatunza watu hawa pamoja nawe, usije ukaubeba mzigo huo peke yako.

18. Sasa waambie watu hivi: Jitakaseni kwa ajili ya kesho; mtakula nyama. Mwenyezi-Mungu amesikia mkilia na kusema kuwa hakuna wa kuwapeni nyama, na kwamba hali yenu ilikuwa nzuri zaidi mlipokuwa Misri. Sasa Mwenyezi-Mungu atawapeni nyama, nanyi sharti muile.

19. Mtakula nyama si kwa muda wa siku moja tu, au mbili, au tano, au kumi au ishirini,

20. bali kwa muda wa mwezi mzima! Mtaila hadi iwatoke puani, mpaka muikinai. Yote hayo ni kwa sababu mmemkataa Mwenyezi-Mungu aliye hapahapa miongoni mwenu, na kulia mbele yake mkisema, ‘Kwa nini tulitoka Misri?’”

21. Lakini Mose alimwambia Mwenyezi-Mungu, “Idadi ya watu ninaowaongoza hapa ni 600,000 waendao kwa miguu, nawe wasema, ‘Nitawapa nyama ya kuwatosha mwezi mzima!’

22. Je, panaweza kuchinjwa kondoo na ng'ombe wa kuwatosheleza? Je, samaki wote baharini wavuliwe kwa ajili yao?”

23. Mwenyezi-Mungu akamjibu Mose, “Je, uwezo wangu umepungua? Utaona basi kama neno langu litakuwa la kweli kwako au la.”

24. Basi, Mose akaenda na kuwajulisha watu yale aliyosema Mwenyezi-Mungu. Kisha, akakusanya wazee sabini kutoka miongoni mwa wazee viongozi nao akawaweka kandokando kuizunguka hema.

25. Hapo, Mwenyezi-Mungu akashuka katika wingu na kuzungumza naye. Halafu akatwaa sehemu ya roho aliyokuwa amempa Mose, akawapa kila mmoja wa wale wazee sabini. Walipoingiwa na roho hiyo, wazee hao walianza kutoa unabii, lakini hawakurudia kufanya hivyo.

26. Wazee wawili kati ya wale sabini waliochaguliwa, Eldadi na Medadi, walikuwa wamebaki kambini wenzao walipokwenda kwenye hema. Roho iliwajia humohumo kambini, wakaanza kutoa unabii mahali walipokuwa.

27. Kijana mmoja alitoka mbio na kumwambia Mose, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.”

Hesabu 11