Danieli 11:25-42 Biblia Habari Njema (BHN)

25. “ ‘Kwa ujasiri mwingi, ataunda jeshi kubwa ili kuushambulia ufalme wa kusini, naye mfalme wa kusini atajibu mashambulizi hayo kwa jeshi kubwa zaidi na lenye nguvu sana. Lakini, mfalme wa kusini hatafaulu kwani mipango ya hila itafanywa dhidi yake.

26. Wale wanaokula pamoja naye, ndio watakaomwangamiza. Watamwangamiza na jeshi lake litafagiliwa mbali na wengi watauawa.

27. Hapo wafalme hao wawili wataketi pamoja mezani kula, lakini kila mmoja anamwazia mwenzake uovu, na kudanganyana. Ila hawatafanikiwa, maana wakati uliopangwa utakuwa bado haujatimia.

28. Mfalme wa kaskazini atarudi nchini mwake akiwa na mali nyingi, lakini nia yake moyoni ni kulitangua agano takatifu. Atafanya apendavyo, kisha atarudi katika nchi yake.

29. “ ‘Katika wakati uliopangwa ataivamia nchi ya kusini kwa mara nyingine, lakini safari hii, mambo yatakuwa tofauti.

30. Meli kutoka Kitimu zitamshambulia, naye atashikwa na hofu. Kisha atarudi nyuma huku amejaa hasira na atalitangua agano takatifu. Hapo atafuata shauri la wale walioasi agano takatifu.

31. Wanajeshi wake watalitia najisi hekalu na ngome zake, watakomesha tambiko za kuteketezwa kila siku na kusimamisha huko hekaluni chukizo haribifu.

32. Atawashawishi kwa hila wale walioasi agano, lakini watu walio waaminifu kwa Mungu wao watasimama imara na kuchukua hatua.

33. Wenye hekima miongoni mwa watu watawafundisha wengi. Hata hivyo, kwa siku kadhaa watauawa kwa upanga au moto, watachukuliwa mateka au kunyanganywa mali zao.

34. Wakati wanapouawa, watapata msaada kidogo, na wengi wanaojiunga nao, watafanya hivyo kwa unafiki.

35. Baadhi ya wenye hekima watauawa, ili wapate kuondolewa uchafu, kutakaswa na kusafishwa, mpaka wakati wa mwisho, ambao sasa bado haujatimia.

36. “ ‘Mfalme atafanya kama apendavyo. Atajitukuza na kujikweza kwamba yeye ni mkuu kuliko miungu yote, na kumkufuru Mungu wa miungu. Ataendelea kufanikiwa mpaka ghadhabu ifikie kikomo chake, kwani yaliyopangwa lazima yatimie.

37. Mfalme huyo hataijali miungu ya wazee wake wala yule anayependwa na wanawake. Ataidharau miungu mingine yote, kwani atajiweka kuwa mkuu kuliko kila mmoja wao.

38. Badala ya miungu hiyo atamheshimu mungu mlinzi wa ngome, ambaye wazee wake kamwe hawakumwabudu, atamtolea dhahabu, fedha na vito vya thamani, na zawadi za thamana kubwa.

39. Atazishughulikia ngome zake kwa msaada wa mungu wa kigeni. Wale wanaomtambua kuwa mfalme, atawatunukia heshima kubwa, atawapa vyeo vikubwa na kuwagawia ardhi kama zawadi.

40. “ ‘Wakati wa mwisho mfalme wa kusini atamshambulia mfalme huyo wa kaskazini. Lakini mfalme wa kaskazini atajibu mashambulio hayo kwa nguvu kama kimbunga, akitumia magari ya farasi, wapandafarasi na meli nyingi. Atazivamia nchi nyingi na kupita katika nchi hizo kama mafuriko ya maji.

41. Ataivamia hata nchi ile tukufu na kuua maelfu ya watu. Lakini nchi za Edomu, Moabu na sehemu kubwa ya Amoni, zitaokoka kutoka mikononi mwake.

42. Wakati atakapozivamia nchi hizo, hata nchi ya Misri haitanusurika.

Danieli 11