1. Siku moja, Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono: Nilimwona Mungu anaumba nzige kundi zima, mara baada ya watu kumaliza kukata nyasi kwa ajili ya wanyama wa mfalme. Wakati huo, nyasi zilikuwa ndio zinaanza kuchipua tena.
2. Niliwaona nzige hao wakila na kumaliza kila jani katika nchi. Ndipo nikasema:“Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi utuhurumie!Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi?Wao ni wadogo mno!”
3. Basi, Bwana Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake,akasema, “Haitakuwa hivyo!”
4. Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono mengine: Nilimwona Bwana Mwenyezi-Mungu akiuita moto wa hukumu ya kuwaadhibu watu. Moto huo uliunguza vilindi vikuu vya bahari, ukaanza kuiteketeza nchi kavu.
5. Ndipo nikasema:“Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, nakusihi uache kuadhibu!Wazawa wa Yakobo watawezaje kuishi?Wao ni wadogo mno!”
6. Basi, Mwenyezi-Mungu akabadili nia yake,akasema: “Hili pia halitatukia.”