11. Shauri langu ni kwamba, uwakusanye kwako watu wote wa Israeli tangu Dani hadi Beer-sheba, upande wa kusini, wawe wengi kama mchanga wa bahari, na wewe mwenyewe binafsi uende vitani.
12. Nasi tutamwendea Daudi mahali popote anapoweza kupatikana na tutamvamia kama umande unavyoiangukia ardhi. Basi, hakuna atakayesalia hata kama atakuwa yeye mwenyewe au watu wake wote walio pamoja naye.
13. Iwapo atakimbilia mji fulani, basi, watu wote wa Israeli wataleta kamba na kuuburuta mji huo, hadi bondeni, kisibaki chochote hata jiwe dogo la mji huo.”
14. Absalomu pamoja na watu wote wa Israeli wakasema, “Shauri la Hushai ni bora kuliko shauri la Ahithofeli.” Wakakataa shauri la Ahithofeli kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alikuwa amepanga kulishinda shauri jema la Ahithofeli ili aweze kumletea Absalomu maafa.
15. Kisha Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari jinsi Ahithofeli na yeye mwenyewe walivyomshauri Absalomu na wazee wa Israeli.