2 Mambo Ya Nyakati 32:18-28 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Maofisa hao waliwaambia kwa sauti kubwa kwa lugha ya Kiebrania watu wa Yerusalemu waliokuwa ukutani, wakikusudia kuwatia hofu na woga ili wauteke mji kwa urahisi.

19. Wakazungumza juu ya Mungu wa Yerusalemu kana kwamba ni miungu ya mataifa mengine; sanamu tu zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu!

20. Hapo mfalme Hezekia na nabii Isaya, mwana wa Amozi, wakamwomba Mungu na kumlilia awasaidie kwa ajili ya mambo haya.

21. Naye Mwenyezi-Mungu akatuma malaika, akaenda na kuwakatilia mbali mashujaa, wanajeshi, makamanda na maofisa katika kambi ya mfalme wa Ashuru. Basi, mfalme wa Ashuru akarejea nchini mwake amejawa aibu. Mara alipoingia ndani ya nyumba ya mungu wake, baadhi ya wanawe mwenyewe wakamuua papo hapo kwa upanga.

22. Kwa njia hii basi, Mwenyezi-Mungu akamwokoa mfalme Hezekia na wakazi wa Yerusalemu kutoka mkono wa Senakeribu mfalme wa Ashuru, na kutoka mkono wa maadui wake wote. Akawapa maisha ya amani na jirani zake wote.

23. Watu wengi sana walikuja wakamletea Mwenyezi-Mungu tambiko huko Yerusalemu, pia wakamletea Hezekia, mfalme wa Yuda zawadi za thamani. Hivyo kutoka wakati huo, akasifiwa sana na mataifa mengine yote.

24. Wakati huo, Hezekia aliugua sana, karibu na kufa. Akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akamjibu na kumpa ishara.

25. Lakini Hezekia hakumtolea Mwenyezi-Mungu shukrani kwa hayo yote aliyomtendea kwa kuwa moyo wake ulikuwa umejaa majivuno. Hii ilisababisha kutaabika kwa Yuda na Yerusalemu.

26. Kwa hiyo ghadhabu ikawa juu yake, juu ya Yuda na juu ya Yerusalemu. Hatimaye Hezekia alinyenyekea akaacha kuwa na moyo uliojaa majivuno; yeye na wakazi wa Yerusalemu walijinyenyekesha kwa hiyo ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu haikuwajia wakati Hezekia alipokuwa hai.

27. Mfalme Hezekia alitajirika sana, akaheshimiwa. Alijitengenezea hazina za fedha, za dhahabu, za vito, za viungo, ngao na za aina zote za vyombo vya thamani kubwa.

28. Aidha, alijijengea mabohari ya kuhifadhia mazao ya nafaka, divai na mafuta, na mazizi kwa ajili ya ng'ombe na mengine kwa ajili ya kondoo.

2 Mambo Ya Nyakati 32