4. Yeye alimtafuta Mungu wa baba yake na kuzitii amri zake, wala hakufuata matendo ya watu wa Israeli.
5. Mwenyezi-Mungu, aliuimarisha ufalme wa Yuda mikononi mwa Yehoshafati, nao watu wote wakamletea zawadi, akatajirika sana na kuheshimika.
6. Alipenda sana moyoni kumtumikia Mwenyezi-Mungu, na zaidi ya hayo, alipaharibu mahali pote pa kuabudia miungu mingine na sanamu za Ashera, mungu wa kike, nchini Yuda.
7. Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wake, Yehoshafati aliwatuma maofisa wafuatao wakafundishe katika miji ya Yuda: Ben-haili, Obadia, Zekaria, Nethaneli na Mikaya.
8. Walawi tisa na Makuhani wawili waliandamana nao. Walawi hao walikuwa Shemaya, Nethania, Zebadia, Asaheli, Shemiramothi, Yehonathani, Adoniya, Tobia na Tob-adoniya; na makuhani walikuwa Elishama na Yehoramu.
9. Walikichukua kitabu cha sheria ya Mwenyezi-Mungu, wakazunguka nacho katika miji yote ya Yuda wakifundisha watu.
10. Mwenyezi-Mungu alizitia hofu falme zote jirani na Yuda, zikaogopa kupigana vita na Yehoshafati.
11. Baadhi ya Wafilisti walimletea Yehoshafati zawadi pamoja na fedha nyingi, na Waarabu wengine nao wakamletea kondoo madume 7,700, na mabeberu 7,700.
12. Kwa hiyo Yehoshafati aliendelea kuwa mkuu zaidi. Alijenga ngome na miji yenye ghala,