1 Mambo Ya Nyakati 15:4-16 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Halafu Daudi akawaita wazawa wa Aroni na Walawi:

5. Kutoka katika ukoo wa Kohathi, wakaja Urieli, pamoja na ndugu zake120 chini ya usimamizi wake;

6. kutoka katika ukoo wa Merari wakaja Asaya pamoja na ndugu zake 220 chini ya usimamizi wake;

7. kutoka katika ukoo wa Gershomu, wakaja Yoeli pamoja na ndugu zake 130 chini ya usimamizi wake;

8. kutoka katika ukoo ya Elisafani, wakaja Shemaya pamoja na ndugu zake 200 chini ya usimamizi wake;

9. kutoka katika ukoo wa Hebroni, wakaja Elieli pamoja na ndugu zake 80 chini ya usimamizi wake;

10. na kutoka katika ukoo wa Uzieli, wakaja Aminadabu pamoja na ndugu zake 112 chini ya usimamizi wake.

11. Daudi akawaita makuhani wawili: Sadoki na Abiathari, na Walawi sita: Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu;

12. akawaambia, “Nyinyi ni viongozi wa koo za Walawi. Jitakaseni pamoja na ndugu zenu, ili mkalilete sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, hadi mahali ambapo nimelitayarishia.

13. Kwa sababu hamkulibeba safari ya kwanza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alituadhibu kwani hatukulitunza kama alivyoagiza.”

14. Basi, makuhani na Walawi wakajitakasa ili wapate kulileta sanduku la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

15. Walawi wakalibeba mabegani mwao wakitumia mipiko yake kama Mose alivyoamuru, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu.

16. Daudi pia aliwaamuru wakuu wa Walawi wachague baadhi ya ndugu zao wawe wakiimba na kupiga ala za muziki: Vinanda, vinubi na matoazi kwa nguvu, ili kutoa sauti za furaha.

1 Mambo Ya Nyakati 15