Yon. 1:1-7 Swahili Union Version (SUV)

1. Basi neno la BWANA lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema,

2. Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.

3. Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa BWANA; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa BWANA.

4. Lakini BWANA alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika.

5. Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi.

6. Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee.

7. Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.

Yon. 1