13. Ee BWANA, tumaini la Israeli, wote wakuachao watatahayarika. Wao watakaojitenga nami wataandikwa katika mchanga, kwa sababu wamemwacha BWANA, kisima cha maji yaliyo hai.
14. Uniponye, Ee BWANA, nami nitaponyeka; uniokoe, nami nitaokoka; kwa maana wewe ndiwe uliye sifa zangu.
15. Tazama, wao waniambia, Neno la BWANA liko wapi? Na lije, basi.
16. Mimi hapa sikufanya haraka kuacha kuwa mchungaji nyuma yako; wala sikuitamani siku ya maradhi ya kufisha; wewe unajua; yaliyotoka midomoni mwangu yalikuwa mbele za uso wako.
17. Usiwe sababu ya hofu kuu kwangu mimi; wewe ndiwe uliye kimbilio langu siku ya uovu.
18. Na waaibike watu wanaoniudhi, lakini nisiaibike mimi; na waone hofu kuu, lakini mimi nisione hofu kuu; ulete juu yao siku ya uovu; uwaangamize maangamizo maradufu.
19. BWANA akaniambia hivi, Enenda ukasimame katika lango la wana wa watu hawa, waingiapo wafalme wa Yuda, na watokeapo, na katika malango yote ya Yerusalemu,
20. ukawaambie, Lisikieni neno la BWANA, enyi wafalme wa Yuda, na Yuda wote, nanyi wenyeji wote wa Yerusalemu, ninyi mwingiao kwa malango haya;
21. BWANA asema hivi, Jihadharini nafsi zenu, msichukue mzigo wo wote siku ya sabato, wala msiulete ndani kwa malango ya Yerusalemu;
22. wala msitoe mzigo katika nyumba zenu siku ya sabato, wala msifanye kazi yo yote; bali itakaseni siku ya sabato, kama nilivyowaamuru baba zenu;
23. lakini hawakusikiliza, wala hawakutega masikio yao, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, ili wasisikilize wala wasipokee mafundisho.
24. Na itakuwa, kama mkinisikiliza mimi kwa bidii, asema BWANA, msiingize mzigo wo wote kwa malango ya mji huu siku ya sabato, bali mkiitakasa siku ya sabato, bila kufanya kazi yo yote siku hiyo;
25. ndipo watakapoingia wafalme na wakuu kwa malango ya mji huu; wataketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kupanda magari na farasi, wao, na wakuu wao, watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; na mji huu utakaa hata milele.
26. Nao watatoka miji ya Yuda, na mahali palipo pande zote za Yerusalemu, na nchi ya Benyamini, na Shefela, na milima, na upande wa Negebu, wakileta sadaka za kuteketezwa, na dhabihu, na sadaka za unga, na ubani, wakileta pia sadaka za shukrani, nyumbani kwa BWANA
27. Lakini kama hamtaki kunisikiliza, kuitakasa siku ya sabato, kutokuchukua mzigo na kuingia kwa malango ya Yerusalemu siku ya sabato; basi, nitawasha moto malangoni mwake, nao utaziteketeza nyumba za enzi za Yerusalemu, wala hautazimika.