Lk. 12:27-38 Swahili Union Version (SUV)

27. Yatafakarini maua jinsi yameavyo; hayatendi kazi wala hayasokoti; nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo.

28. Basi, ikiwa Mungu huvika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatawatendea ninyi zaidi, enyi wa imani haba?

29. Ninyi msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa; wala msifanye wasiwasi,

30. kwa maana, hayo yote ndiyo watafutayo mataifa ya duniani, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mna haja na hayo.

31. Bali utafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa.

32. Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme.

33. Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu.

34. Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu.

35. Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka;

36. nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.

37. Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia.

38. Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwakuta hivi, heri watumwa hao.

Lk. 12