1. Mnamo mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario wa Persia, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia, mjukuu wa Ido:
2. “Mimi Mwenyezi-Mungu nilichukizwa sana na wazee wenu.
3. Basi, waambie watu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: Nirudieni, nami nitawarudieni nyinyi.
4. Msiwe kama wazee wenu ambao manabii waliwaambia waachane na mienendo yao miovu na matendo yao mabaya, lakini wao hawakunisikiliza wala hawakunitii mimi Mwenyezi-Mungu.
5. Wazee wenu, wako wapi? Na manabii, je, wanaishi milele?
6. Je, wazee wenu hawakupata adhabu kwa sababu ya kukataa maagizo yangu na amri nilizowapa kwa njia ya watumishi wangu manabii? Wakati huo, wao walitubu na kusema kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nilikusudia kuwatenda kulingana na mienendo yao na matendo yao, na kweli ndivyo nilivyowatenda.”
7. Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi wa Shebati, mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia mimi nabii Zekaria mwana wa Berekia, mjukuu wa Ido, kama ifuatavyo:
8. Wakati wa usiku, nilimwona malaika amepanda farasi mwekundu. Malaika huyo alikuwa amesimama bondeni, katikati ya miti ya mihadasi. Nyuma yake kulikuwa na farasi wengine wekundu, wa kijivujivu na weupe.
9. Basi, nikamwuliza, “Bwana, Farasi hawa wanamaanisha nini?” Malaika huyo aliyeongea nami akaniambia, “Nitakuonesha hao farasi wanamaanisha nini.