4. Sababu ya kuwatahiri Waisraeli ni hii: Waisraeli wote, wanaume, waliotoka Misri ambao walikuwa na umri wa kwenda vitani, wote walifariki safarini jangwani baada ya kutoka nchini Misri.
5. Hao wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini wale wote waliozaliwa safarini huko jangwani baada ya kutoka Misri, walikuwa bado hawajatahiriwa.
6. Waisraeli walisafiri kwa muda wa miaka arubaini nyikani hata wanaume wote waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakaangamia kwa kuwa hawakusikiliza aliyosema Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu alikuwa amewaapia watu hao kwamba hawataiona nchi ile inayotiririka maziwa na asali ambayo yeye aliwaapia baba zao kuwa atawapa.
7. Kwa hiyo ilikuwa ni watoto wa watu hao ambao Mwenyezi-Mungu aliwakuza badala yao, hao ndio Yoshua aliwatahiri, kwani hawakuwa wametahiriwa wakati ule walipokuwa safarini jangwani.
8. Wanaume wote walipokwisha tahiriwa walikaa katika sehemu zao humo kambini mpaka walipopona.
9. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Leo hii nimewaondoleeni ile aibu ya Misri.” Hivyo mahali hapo pakaitwa Gilgali mpaka hivi leo.
10. Waisraeli walipokuwa wamepiga kambi huko Gilgali waliadhimisha sikukuu ya Pasaka jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi katika tambarare za Yeriko.
11. Kesho yake, yaani baada ya Pasaka, walikula mikate isiyotiwa chachu na bisi kutokana na mazao ya nchi ile.
12. Basi, tangu siku hiyo walipokula mazao ya nchi hiyo Waisraeli hawakupata mana tena. Tangu mwaka huo Waisraeli walikula mazao ya nchi ya Kanaani.
13. Siku moja Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, ghafla aliona mtu mmoja amesimama mbele yake na upanga uliofutwa mkononi mwake. Yoshua akamwendea, akamwuliza, “Je, wewe ni wetu au ni wa adui zetu?”