3. Mimi Mungu nilimwondoa babu yenu Abrahamu kutoka huko ngambo ya mto Eufrate na kumleta hapa Kanaani, ambako nilimpatia wazawa wengi. Nilimpa Isaka,
4. naye Isaka nikampa Yakobo na Esau. Nilimpa Esau milima ya Seiri aimiliki. Lakini Yakobo na watoto wake walikwenda Misri.
5. Baadaye niliwatuma Mose na Aroni, nikailetea nchi ya Misri mapigo, na baadaye nikawatoa nyinyi nchini humo.
6. Niliwatoa wazee wenu kutoka Misri na kuwaleta hadi kwenye bahari ya Shamu. Wamisri waliwafuatia wakiwa na magari na askari wapandafarasi.
7. Waisraeli waliponililia mimi Mwenyezi-Mungu, niliweka giza kati yao na Wamisri na kuifanya bahari iwafunike Wamisri. Nyinyi wenyewe mlijionea yale niliyowatendea Wamisri. Mliishi jangwani muda mrefu.
8. Kisha niliwaongoza hadi katika nchi ya Waamori ambao waliishi upande mwingine wa mto Yordani. Walipigana nanyi, lakini mimi niliwapeni ushindi juu yao mkawaangamiza na kuiteka nchi yao.
9. Naye Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, akaja na kuwashambulia Waisraeli. Akamwalika Balaamu mwana wa Beori aje kuwalaani nyinyi.
10. Lakini mimi sikumsikiliza Balaamu, naye ikambidi kuwabariki, nami nikawaokoa nyinyi mikononi mwa Balaki.
11. Halafu mkavuka mto Yordani, mkafika Yeriko. Wakazi wa Yeriko walipigana nanyi, hali kadhalika na Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi. Hao mimi nikawatia mikononi mwenu.