15. Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwachukua uhamishoni watu waliokuwa wamebakia mjini na wale waliokuwa wamejisalimisha kwa mfalme wa Babuloni pamoja na mafundi.
16. Lakini Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwaacha baadhi ya watu waliokuwa maskini kabisa nchini, wawe watunza mizabibu na wakulima.
17. Wakaldayo walivunja vipandevipande nguzo za shaba nyeusi ambazo zilikuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu pamoja na vikalio na birika kubwa la shaba nyeusi lililokuwamo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaichukua shaba nyeusi yote mpaka Babuloni.
18. Kadhalika, walichukua vyungu, sepetu, mikasi, makarai, vijiko vikubwa na vyombo vyote vya shaba nyeusi vilivyotumiwa katika huduma ya hekalu.
19. Pia kapteni wa walinzi wa mfalme alichukua vibakuli, vyetezo, mabirika, vyungu, vinara vya taa, vijiko vikubwa na mabakuli ya sadaka za vinywaji, vyombo hivyo vikiwa vya dhahabu au vya fedha.
20. Kuhusu vitu Solomoni alivyotengeneza: Nguzo mbili, birika kubwa moja na sanamu za fahali kumi na mbili za shaba nyeusi ambazo zilikuwa chini ya hilo birika kubwa pamoja na vikalio, shaba nyeusi ya vitu hivi vyote ilikuwa na uzito mwingi sana.
21. Kila moja ya nguzo hizo mbili ilikuwa na urefu wa mita 8, mzingo wake mita 5.25, na unene wa milimita 75, zote zilikuwa wazi ndani.