17. Hapo Yeremia akamwambia Sedekia: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Kama ukijitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, utayaokoa maisha yako na mji hautateketezwa kwa moto; nawe pamoja na jamaa yako mtaendelea kuishi.
18. Lakini usipojitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, basi, mji huu utatekwa na Wakaldayo nao watauteketeza kwa moto, nawe hutaweza kujiepusha mikononi mwao.”
19. Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, “Nawaogopa Wayahudi waliokimbilia kwa Wakaldayo. Huenda nikakabidhiwa kwao, wakanitesa.”
20. Yeremia akamjibu, “Hutakabidhiwa kwao. Wewe sasa tii anachosema Mwenyezi-Mungu, kama ninavyokuambia, na mambo yote yatakuendea vema, na maisha yako yatasalimika.
21. Lakini kama ukikataa kujitoa mwenyewe na kujitia mikononi mwao, haya ndiyo maono ambayo Mwenyezi-Mungu amenionesha.
22. Katika maono hayo, niliona wanawake waliobaki katika ikulu ya mfalme wa Yuda wakipelekwa kwa maofisa wa mfalme wa Babuloni, nao walikuwa wakisema hivi:‘Marafiki zako uliowaamini wamekudanganya,nao wamekushinda;kwa kuwa miguu yako imezama matopeni,wamekugeuka na kukuacha.’
23. Wake zako wote na watoto wako watapelekwa kwa Wakaldayo, nawe mwenyewe hutanusurika. Utachukuliwa mateka na mfalme wa Babuloni na mji huu utateketezwa kwa moto.”
24. Sedekia akamwambia Yeremia: “Mtu yeyote asijue habari hizi, nawe hutauawa.
25. Kama viongozi wakisikia kuwa nimeongea nawe, kisha wakaja na kukuambia, ‘Hebu tuambie, ulizungumza nini na mfalme. Usitufiche chochote nasi hatutakuua’;