Yeremia 33:12-18 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Mahali hapa ambapo ni jangwa bila watu wala wanyama, na katika miji yake yote, patakuwa na malisho ambayo wachungaji watalisha makundi yao ya kondoo.

13. Katika miji ya nchi yenye milima, katika miji ya Shefela na katika miji ya jangwa la Negebu, katika nchi ya Benyamini, kandokando ya mji wa Yerusalemu na katika miji ya Yuda, watu watahesabu tena kondoo wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

14. Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo nitatimiza ahadi yangu niliyofanya na watu wa Israeli na watu wa Yuda.

15. Katika siku hizo, naam, wakati huo, nitachipusha chipukizi mwadilifu wa uzao wa Daudi. Chipukizi huyo atatekeleza haki na uadilifu katika nchi.

16. Wakati huo nchi ya Yuda itaokolewa na mji wa Yerusalemu utakuwa salama. Na mji huo utaitwa ‘Mwenyezi-Mungu ni Ukombozi Wetu’.

17. Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hapatakosekana kamwe mzawa wa Daudi atakayetawala Israeli.

18. Kadhalika nao makuhani wa ukoo wa Lawi watakuwapo daima kunihudumia wakinitolea sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka na kunitolea tambiko milele.”

Yeremia 33