21. Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Mimi sikuwatuma hao manabii,lakini wao walikwenda mbio;sikuwaambia kitu chochote,lakini wao walitabiri!
22. Kama wangalihudhuria baraza langu,wangaliwatangazia watu wangu maneno yangu,wakawageuza kutoka katika njia zao mbovu,na kutoka katika matendo yao maovu.
23. “Mimi ni Mungu aliye karibu, si Mungu aliye mbali.
24. Je, mtu aweza kujificha mahali pa siri hata nisiweze kumwona? Hamjui kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nipo kila mahali, mbinguni na duniani? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
25. Mimi nimeyasikia maneno waliyosema hao manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, wakisema, ‘Nimeota ndoto, nimeota ndoto!’
26. Itakuwa hivyo mpaka lini? Hao manabii wataendelea mpaka lini kupotoka moyo; kutabiri uongo na udanganyifu wa mioyo yao wenyewe?
27. Kwa ndoto zao hizo wanapanga kuwafanya watu wangu wanisahau mimi kama baba zao walivyonisahau, wakamwendea Baali!
28. Nabii aliyeota ndoto, na aitangaze ndoto yake, lakini yeye aliye na neno langu, na alitangaze kwa uaminifu. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema, makapi si sawa na ngano!
29. Neno langu ni kama moto; ni kama nyundo ipasuayo miamba vipandevipande.
30. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nitawashambulia manabii ambao wanaibiana maneno yangu.
31. Kweli mimi Mwenyezi-Mungu nasema, nitawashambulia manabii wanaoropoka maneno yao wenyewe na kusema, ‘Mwenyezi-Mungu asema’.
32. Naam, mimi Mwenyezi-Mungu nasema kuwa nitawashambulia manabii wanaotabiri ndoto zao za uongo kwa watu wangu, na kuwapotosha kwa uongo wao na kuropoka kwao. Mimi sikuwatuma wala kuwaamuru waende; kwa hiyo hawatawafaa watu hao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”