Yeremia 1:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Yafuatayo ni maneno ya Yeremia mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani wa mji wa Anathothi, katika nchi ya Benyamini.

2. Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia mnamo mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda.

3. Lilimjia tena wakati Yehoyakimu mwana wa Yosia, alipokuwa mfalme wa Yuda. Yeremia aliendelea kupata neno la Mwenyezi-Mungu hadi mwishoni mwa mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda. Mnamo mwezi wa tano wa mwaka huo, watu wa Yerusalemu walipelekwa uhamishoni.

4. Mwenyezi-Mungu aliniambia neno lake:

5. “Kabla hujachukuliwa mimba, mimi nilikujua,kabla hujazaliwa, mimi nilikuweka wakfu;nilikuteua uwe nabii kwa mataifa.”

6. Nami nikajibu, Aa! Bwana Mwenyezi-Mungu,mimi sijui kusema, kwa kuwa bado ningali kijana.

7. Lakini Mwenyezi-Mungu akaniambia,“Usiseme kwamba wewe ni kijana bado.Utakwenda kwa watu wote nitakaokutuma kwao,na yote nitakayokuamuru utayasema.

8. Wewe usiwaogope watu hao,kwa maana niko pamoja nawe kukulinda.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

9. Kisha Mwenyezi-Mungu akaunyosha mkono wake, akagusa kinywa changu, akaniambia,“Tazama nimeyatia maneno yangu kinywani mwako.

10. Leo nimekupa mamlaka juu ya mataifa na falme,uwe na mamlaka ya kungoa na kubomoa,mamlaka ya kuharibu na kuangamiza,mamlaka ya kujenga na ya kupanda.”

Yeremia 1