10. Kisha Mose akachukua mafuta ya kupaka, akaipaka ile maskani na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake akaviweka wakfu.
11. Alinyunyiza sehemu ya mafuta hayo juu ya madhabahu mara saba, akaipaka mafuta na vyombo vyake vyote, birika na tako lake, kuviweka wakfu.
12. Vilevile Mose akampaka Aroni mafuta kichwani ili kumweka wakfu.
13. Kisha Mose akawaleta wana wa Aroni akawavika joho na kuwafunga mikanda viunoni, na kuwavisha kofia kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.
14. Kisha Mose akamleta ng'ombe wa sadaka ya kuondoa dhambi, naye Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa cha ng'ombe huyo.
15. Mose akamchinja huyo ng'ombe, akachukua damu akazipaka pembe za madhabahu pande zote kwa kidole chake kuitakasa. Kisha akachukua damu iliyobaki akaimwaga chini kwenye tako la madhabahu ambayo aliweka wakfu kwa kuifanyia ibada ya upatanisho.
16. Kisha, akachukua mafuta yote yaliyokuwa kwenye matumbo yake, sehemu bora ya ini pamoja na figo zote mbili na mafuta yake na kuviteketeza juu ya madhabahu.
17. Lakini nyama ya ng'ombe huyo, ngozi yake na mavi yake, akaviteketeza kwa moto nje ya kambi kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.
18. Kisha, Mose akamleta kondoo dume wa sadaka ya kuteketezwa. Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa cha kondoo huyo.
19. Mose akamchinja na damu ya kondoo huyo akairashia madhabahu pande zake zote.
20. Alimkata huyo kondoo vipandevipande, akaviteketeza pamoja na kichwa chake na mafuta yake.
21. Baada ya matumbo na miguu kuoshwa kwa maji, Mose aliviteketeza vyote juu ya madhabahu pamoja na sehemu nyingine za huyo kondoo kama sadaka ya kuteketezwa. Hiyo ni sadaka itolewayo kwa moto, yenye harufu ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. Mose alifanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.
22. Kisha akamleta kondoo dume mwingine, kwa ajili ya kuweka wakfu. Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa cha kondoo huyo.
23. Mose akamchinja. Akachukua damu ya kondoo huyo na kumpaka Aroni kwenye ncha ya sikio lake la kulia, kidole gumba cha mkono wake wa kulia na cha mguu wake wa kulia.
24. Wanawe Aroni nao wakaja, naye Mose akawapaka kiasi cha damu kwenye ncha za masikio yao ya kulia, vidole gumba vya mikono yao ya kulia na kwenye vidole gumba vya miguu yao ya kulia. Damu nyingine akainyunyizia madhabahu pande zake zote.
25. Kisha, akachukua mafuta yote, mkia pamoja na mafuta yake, mafuta yote yanayofunika matumbo, sehemu bora ya ini, pamoja na figo zote mbili, mafuta yake na paja la mguu wa kulia wa nyuma wa huyo kondoo dume.