Walawi 8:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

2. “Mwite Aroni na wanawe wakutane mbele ya mlango wa hema la mkutano; chukua mavazi matakatifu, mafuta ya kupaka, ng'ombe wa sadaka ya kuondolea dhambi, kondoo madume wawili, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu.

3. Kisha, ikusanye jumuiya yote ya Waisraeli mbele ya mlango wa hema la mkutano.”

4. Mose akafanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, akaikusanya jumuiya yote mbele ya mlango wa hema la mkutano.

5. Mose akaiambia jumuiya yote hivi: “Lifuatalo ni jambo ambalo Mwenyezi-Mungu ameamuru lifanywe.”

6. Hapo Mose akawaleta Aroni na wanawe na kuwatawadha.

7. Kisha akamvika Aroni joho na kuifunga kwa mkanda, akamvika kanzu, akamvalisha kizibao na kukifunga kiunoni mwake kwa mkanda uliofumwa kwa ustadi.

8. Kisha akaweka kifuko kifuani pa Aroni na ndani ya kifuko hicho akatia mawe ya kauli.

9. Halafu akamvika Aroni kilemba na upande wa mbele wa kilemba hicho akaweka pambo la dhahabu, taji takatifu, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru.

10. Kisha Mose akachukua mafuta ya kupaka, akaipaka ile maskani na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake akaviweka wakfu.

Walawi 8