6. Wanaoruhusiwa kula sadaka hiyo ni wanaume wa ukoo wa makuhani peke yao; ni sadaka takatifu kabisa. Italiwa katika mahali patakatifu.
7. Sheria ni moja kuhusu sadaka ya kuondoa hatia na sadaka ya kuondoa dhambi: Kuhani anayefanya ibada ya upatanisho ndiye atakayeichukua.
8. Kuhani anayetoa sadaka ya kuteketezwa ya mtu yeyote, atachukua ngozi ya mnyama aliyetolewa.
9. Sadaka yoyote ya nafaka iliyookwa jikoni au katika sufuria au katika kikaango itakuwa mali ya kuhani anayeitoa.
10. Kila sadaka ya nafaka, iwe imechanganywa na mafuta au kavu, itakuwa ya wazawa wa Aroni, na wote wagawiwe kwa sawa.
11. “Ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka za amani ambazo mtu aweza kumtolea Mwenyezi-Mungu.
12. Ikiwa mtu anatoa sadaka hiyo ya kumshukuru Mungu, basi, ataitoa pamoja na maandazi yasiyotiwa chachu yaliyopakwa mafuta, mikate myembamba iliyopakwa mafuta na maandazi ya unga laini uliochanganywa na mafuta.
13. Pamoja na sadaka hiyo yake ya amani ya kumshukuru Mungu, ataleta maandazi yaliyotiwa chachu.
14. Kutokana na maandazi hayo, atamtolea Mwenyezi-Mungu andazi moja kutoka kila sadaka; maandazi hayo yatakuwa yake kuhani anayeirashia madhabahu damu ya sadaka za amani.
15. Nyama ya sadaka hiyo ya amani ya kumshukuru Mungu italiwa siku hiyohiyo inapotolewa; hataacha hata sehemu yake hadi asubuhi.
16. Lakini kama sadaka hiyo ya amani ni ya nadhiri au ya hiari, italiwa siku hiyohiyo inapotolewa na sehemu nyingine yaweza kuliwa kesho yake.