Walawi 4:22-33 Biblia Habari Njema (BHN)

22. “Ikiwa mtawala ametenda dhambi bila kukusudia kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, na hivyo akawa na hatia,

23. mara akijulishwa dhambi hiyo aliyotenda, ataleta sadaka yake ya beberu asiye na dosari.

24. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha beberu na kumchinjia mahali wanapochinjia sadaka za kuteketezwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi.

25. Kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka.

26. Mafuta yote ya beberu huyo atayateketeza madhabahuni, kama afanyavyo na mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani. Kwa hiyo kuhani atamfanyia mtawala ibada hiyo ya upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa.

27. “Kama mtu wa kawaida ametenda dhambi bila kukusudia, kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu na hivyo akawa na hatia,

28. mara atakapojulishwa kuwa ametenda dhambi, ataleta sadaka ya mbuzi jike asiye na dosari kwa ajili ya kuondoa dhambi aliyotenda.

29. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mbuzi huyo wa sadaka ya kuondoa dhambi, na kumchinjia mahali wanapochinjia wanyama wa sadaka za kuteketezwa.

30. Kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu iliyobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu.

31. Mafuta yote ya mbuzi huyo atayaondoa kama aondoavyo mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, naye kuhani atayateketeza madhabahuni, na harufu yake nzuri itampendeza Mwenyezi-Mungu. Basi, kuhani atamfanyia huyo mtu hiyo ibada ya upatanisho, naye atasamehewa.

32. “Ikiwa mtu huyo ataleta mwanakondoo kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, basi, ataleta mwanakondoo jike asiye na dosari.

33. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mwanakondoo huyo wa sadaka ya kuondoa dhambi, na kumchinjia mahali pale wanapochinjia wanyama wa sadaka za kuteketezwa.

Walawi 4