1. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
2. “Waambie Waisraeli hivi: Katika sikukuu zangu mimi Mwenyezi-Mungu ambazo zimepangwa mtakuwa na mkutano mtakatifu. Sikukuu ambazo nimepanga ni hizi:
3. Kutakuwa na siku sita za kufanya kazi. Lakini siku ya saba ni Sabato; siku hiyo ni ya mapumziko rasmi, hamtafanya kazi na mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo ya saba hamtafanya kazi; hiyo ni Sabato ambayo ni wakfu kwangu mimi Mwenyezi-Mungu katika makao yenu yote.
4. “Sikukuu zangu nyingine mimi Mwenyezi-Mungu ambazo mtakuwa na mkutano mtakatifu zitafanyika katika nyakati zifuatazo zilizopangwa.
5. “Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza mtaadhimisha kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu sikukuu ya Pasaka.
6. Siku ya kumi na tano ya mwezi huohuo, sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu itaanza. Kwa muda wa siku saba, mtakula mikate isiyotiwa chachu.
7. Katika siku ya kwanza mtakuwa na mkutano mtakatifu. Siku hiyo msifanye kazi.
8. Kwa muda wa siku hizo zote saba mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa kwa moto. Katika siku ya saba mtafanya mkutano mtakatifu. Msifanye kazi.”
9. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
10. “Waambie Waisraeli hivi: Mtakapoingia katika nchi ambayo ninawapeni mkavuna mazao yake, mtamletea kuhani mganda wa mavuno ya kwanza.
11. Kuhani atafanya nayo ishara ya kunitolea siku inayofuata siku ya Sabato ili mpate kukubaliwa.
12. Siku hiyo mnapofanya ishara ya kutoa huo mganda mbele yangu mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa ya mwanakondoo dume wa mwaka mmoja asiye na dosari.
13. Pamoja na sadaka hiyo, mtatoa sadaka ya nafaka ya kilo mbili za unga laini uliochanganywa na mafuta ambayo mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu kwa moto, na harufu yake itanipendeza. Sadaka yake ya kinywaji ni lita moja ya divai.
14. Kabla ya siku hiyo ya kuniletea mimi Mungu wenu sadaka hiyo, hamruhusiwi kula mazao ya kwanza ya mavuno yenu, yawe mabichi, yamekaangwa au yemeokwa kuwa mikate. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu mahali popote mtakapoishi.
15. “Mtahesabu majuma saba kamili tangu siku ile inayofuata Sabato ile ambapo mtaleta mganda wa sadaka ya kunitolea kwa ishara mimi Mwenyezi-Mungu.