1. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waambie makuhani, wana wa Aroni, kwamba pasiwe na mtu yeyote miongoni mwao atakayejitia najisi kwa kugusa maiti ya watu wa jamaa yake,
2. isipokuwa kama ni maiti ya ndugu yake wa karibu, yaani mama yake, baba yake, mwanawe, binti yake, ndugu yake
3. au dada yake ambaye (aliye wa jamaa yake ya karibu), naye hajaolewa bado.
4. Yeye, akiwa mwenye madaraka katika jamaa yake, asijitie unajisi.
5. Wazawa wa Aroni kamwe wasijinyoe upara kuomboleza wala wasikate pembe za ndevu zao wala kujichanja chale mwilini.
6. Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao wala wasilikufuru jina la Mungu wao. Maana wao ndio wanaotolea zile sadaka anazopewa Mwenyezi-Mungu kwa moto yaani chakula cha Mungu. Basi, ni lazima wawe watakatifu.
7. Kwa kuwa kuhani amewekwa wakfu kwa Mungu wake, kamwe asioe kahaba, wala mwanamke asiye bikira wala aliyepewa talaka.
8. Utamtambua kuhani kuwa aliyewekwa wakfu, maana yeye ndiye anayetoa sadaka ya mkate wa Mungu wako; utamtambua kuwa mtakatifu, maana mimi Mwenyezi-Mungu ninayekuweka wewe wakfu, ni mtakatifu.