Walawi 16:19-30 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Atainyunyizia madhabahu hiyo damu kwa kidole chake mara saba na hivyo kuiweka wakfu na kuitakasa unajisi wote wa watu wa Israeli.

20. “Baada ya Aroni kumaliza kupatakasa mahali patakatifu, hema la mkutano na madhabahu, ndipo atamtoa yule beberu kwa ajili ya Azazeli, akiwa hai.

21. Aroni ataweka mikono yake juu ya kichwa cha huyo beberu hai na kuuungama juu yake dhambi zote za watu wa Israeli, makosa yao yote na dhambi zao zote, ili kumwajibisha huyo. Kisha atamwacha huyo beberu aende jangwani akipelekwa huko na mtu yeyote anayejitoa kwa hiari.

22. Atamwacha huyo beberu aende jangwani, mahali pasipokuwa na watu, akiwa ameyachukua maovu yao yote.

23. “Kisha Aroni atarudi ndani ya hema la mkutano, atavua yale mavazi aliyovaa alipoingia mahali patakatifu sana na kuyaacha humo.

24. Ataoga humo ndani katika mahali patakatifu na kuvaa mavazi yake. Atatoka na kutoa sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka ya kuteketezwa ya watu wa Israeli, ili kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote.

25. Mafuta ya sadaka ya kuondoa dhambi atayateketeza juu ya madhabahu.

26. Yule mtu aliyempeleka yule beberu kwa Azazeli kwanza atayafua mavazi yake na kuoga ndipo atakapoweza kuingia kambini.

27. Yule fahali na mbuzi waliotolewa sadaka ya kuondoa dhambi ambao damu yao ilipelekwa mahali patakatifu sana ili kufanya ibada ya upatanisho, watapelekwa nje ya kambi na kuteketezwa. Ngozi zao, nyama na mavi yao, vyote vitateketezwa.

28. Yule mtu atakayewateketeza atayafua mavazi yake na kuoga, ndipo atakapoweza kuingia kambini.

29. “Hili ni sharti ambalo mnapaswa kulifuata milele: Siku ya kumi ya mwezi wa saba, nyinyi wenyewe na hata wageni wanaoishi miongoni mwenu, ni lazima mfunge siku hiyo na kuacha kufanya kazi.

30. Mtafanya hivyo kwa sababu siku hiyo ndiyo siku ambayo mtafanyiwa ibada ya upatanisho, msafishwe dhambi zenu, nanyi mtakuwa safi mbele ya Mwenyezi-Mungu.

Walawi 16