Walawi 15:22-33 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Mtu yeyote atakayegusa kitu chochote anachokalia mwanamke huyo ni lazima ayafue mavazi yake na kuoga kwa maji, naye atakuwa najisi mpaka jioni.

23. Mwanamume yeyote atakayegusa kitu chochote alicholalia au kukalia huyo mwanamke, atakuwa najisi mpaka jioni.

24. Kama mwanamume akilala na mwanamke huyo na damu ya huyo mwanamke ikamdondokea huyo mwanamume, basi, mwanamume huyo atakuwa najisi kwa muda wa siku saba. Kitanda chochote atakacholalia huyo mwanamume kitakuwa najisi.

25. “Kama mwanamke anatokwa na damu kwa muda wa siku nyingi kuliko ilivyo kawaida au anatokwa damu wakati usio wa majira yake ya kutokwa damu, basi, ataendelea kuwa najisi muda wote damu inapomtoka.

26. Kitanda chochote anacholalia wakati huo au kiti chochote anachokalia, kitakuwa najisi sawa kama wakati wa unajisi wake wa kutokwa damu.

27. Mtu yeyote atakayegusa vitu hivyo, atakuwa najisi na ni lazima ayafue mavazi yake na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

28. Baada ya kukauka damu yake mwanamke huyo atangoja hadi siku saba ili kuwa safi; na baada ya muda huo atakuwa safi.

29. Siku ya nane atachukua hua wawili au makinda mawili ya njiwa na kumletea kuhani mlangoni mwa hema la mkutano.

30. Kuhani atamtoa mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Hivyo kuhani atamfanyia huyo mwanamke ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumwondolea unajisi wake wa kutokwa damu.

31. “Ndivyo mtakavyowatahadharisha Waisraeli na unajisi wao, wasije wakaikufuru maskani yangu takatifu iliyo miongoni mwao wakiingia humo na unajisi wao; wakifanya hivyo watauawa.”

32. Hiyo ndiyo sheria kuhusu mwanamume anayetokwa na usaha na anayetokwa na shahawa na kuwa najisi.

33. Sheria hiyo yamhusu pia mwanamke anayetokwa damu na kuwa najisi. Sheria hiyo yamhusu mwanamume au mwanamke yeyote anayetokwa na chochote na pia yahusu mwanamume anayelala na mwanamke ambaye ni najisi.

Walawi 15