Walawi 14:27-37 Biblia Habari Njema (BHN)

27. Kisha atamnyunyizia huyo mtu kwa kidole chake cha kulia kiasi cha hayo mafuta yaliyomo katika kiganja chake cha kushoto mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu.

28. Kuhani atampaka huyo mtu anayetakaswa mafuta katika ncha ya sikio lake la kulia, katika kidole gumba cha mkono wake wa kulia, na kidole gumba cha mguu wake wa kulia. Atampaka mahali pale ambapo alimpaka ile damu ya sadaka ya kuondoa hatia.

29. Mafuta yanayosalia mkononi mwake atampaka huyo mtu kichwani, ili kumfanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu.

30. Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale hua au njiwa wawili kadiri mtu huyo anavyoweza kuleta.

31. Hua atakuwa kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Pamoja na hao, atatoa sadaka ya nafaka; naye kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu.

32. Huo ndio mwongozo kuhusu mtu mwenye ukoma asiyeweza kutoa sadaka za kumtakasa.”

33. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni,

34. “Mtakapoingia katika nchi ya Kanaani ambayo ninawapa kuwa milki yenu, nami nikafanya namna ya upele wa ukoma uote katika ukuta wa nyumba fulani katika nchi mtakayoimiliki,

35. basi, mwenye nyumba hiyo ni lazima amwambie kuhani kwamba namna ya upele wa ukoma umeonekana katika nyumba yake.

36. Kuhani ataamuru vitu vyote ndani ya nyumba hiyo vitolewe kabla yeye mwenyewe hajaanza uchunguzi wake; visije vyote kutangazwa kuwa najisi. Kisha kuhani ataingia kuiangalia nyumba hiyo.

37. Atauchunguza upele huo; kama upele huo umeonekana ukutani na umesababisha madoa ya rangi ya kijani kibichi au nyekundu na kuonekana kuwa yamepenya ndani ya kuta,

Walawi 14