22. Ataleta pia hua wawili au makinda mawili ya njiwa kadiri anavyoweza mmoja atakuwa kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.
23. Siku ya nane atamletea kuhani vitu hivyo mbele ya mlango wa hema la mkutano kwa ajili ya utakaso wake mbele ya Mwenyezi-Mungu.
24. Kuhani atamchukua huyo mwanakondoo dume wa sadaka ya kuondoa hatia pamoja na yale mafuta theluthi moja ya lita na kufanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu.
25. Atamchinja huyo mwanakondoo dume wa sadaka ya kuondoa hatia. Kuhani atachukua kiasi cha damu na kumpaka huyo mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia, katika kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia.
26. Kuhani atatia kiasi cha mafuta hayo katika kiganja cha mkono wake wa kushoto.
27. Kisha atamnyunyizia huyo mtu kwa kidole chake cha kulia kiasi cha hayo mafuta yaliyomo katika kiganja chake cha kushoto mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu.
28. Kuhani atampaka huyo mtu anayetakaswa mafuta katika ncha ya sikio lake la kulia, katika kidole gumba cha mkono wake wa kulia, na kidole gumba cha mguu wake wa kulia. Atampaka mahali pale ambapo alimpaka ile damu ya sadaka ya kuondoa hatia.
29. Mafuta yanayosalia mkononi mwake atampaka huyo mtu kichwani, ili kumfanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu.
30. Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale hua au njiwa wawili kadiri mtu huyo anavyoweza kuleta.
31. Hua atakuwa kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Pamoja na hao, atatoa sadaka ya nafaka; naye kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu.
32. Huo ndio mwongozo kuhusu mtu mwenye ukoma asiyeweza kutoa sadaka za kumtakasa.”
33. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni,
34. “Mtakapoingia katika nchi ya Kanaani ambayo ninawapa kuwa milki yenu, nami nikafanya namna ya upele wa ukoma uote katika ukuta wa nyumba fulani katika nchi mtakayoimiliki,
35. basi, mwenye nyumba hiyo ni lazima amwambie kuhani kwamba namna ya upele wa ukoma umeonekana katika nyumba yake.
36. Kuhani ataamuru vitu vyote ndani ya nyumba hiyo vitolewe kabla yeye mwenyewe hajaanza uchunguzi wake; visije vyote kutangazwa kuwa najisi. Kisha kuhani ataingia kuiangalia nyumba hiyo.
37. Atauchunguza upele huo; kama upele huo umeonekana ukutani na umesababisha madoa ya rangi ya kijani kibichi au nyekundu na kuonekana kuwa yamepenya ndani ya kuta,
38. basi, kuhani atatoka nje mlangoni na kuifunga nyumba hiyo kwa muda wa siku saba.