Walawi 13:8-23 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Kuhani atamwangalia tena, na kama ule upele umeenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; huo ni ukoma.

9. “Kama mtu ameshikwa na ukoma, ataletwa kwa kuhani.

10. Kuhani atamwangalia na kama kuna uvimbe mweupe ambao umezifanya nywele zake ziwe nyeupe na uvimbe huo umegeuka kuwa kidonda kibichi,

11. huo ni ukoma wa muda mrefu. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Hakuna haja ya kumweka mtu huyo kwa uchunguzi kwani yu najisi tayari.

12. Kama ukoma umemshika na umeenea mwili mzima, toka utosini hadi nyayoni kama atakavyoona kuhani,

13. hapo kuhani atamwangalia. Kuhani akiona kuwa ukoma umemwenea mwili mzima, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi kwa sababu mwili umegeuka kuwa mweupe na hivyo mtu huyo yu safi.

14. Lakini kukionekana mwilini mwa mtu huyo kidonda kibichi, basi, mtu huyo atakuwa najisi.

15. Kuhani ataangalia hicho kidonda kibichi na kumtangaza kuwa ni najisi kwa sababu huo ni ukoma.

16. Lakini hicho kidonda kikigeuka tena kuwa cheupe, mtu huyo atarudi kwa kuhani.

17. Kuhani atamwangalia na akiona kuwa kimegeuka kuwa cheupe, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi.

18. “Kama mtu ameshikwa na jipu, nalo limepona,

19. lakini mahali pale lilipokuwa jipu pamegeuka kuwa uvimbe mweupe au kuwa pekundu lakini peupe kiasi, ni lazima kumwonesha kuhani.

20. Kuhani atamwangalia huyo mtu. Kuhani akiona pamegeuka kuwa na shimo na nywele za mahali hapo zimegeuka kuwa nyeupe, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; huo ni ugonjwa wa ukoma ambao umetokana na jipu.

21. Lakini kama kuhani atamwangalia huyo mtu na kuona kuwa nywele za mahali hapo si nyeupe na wala hakuna shimo, ila pamefifia, basi, atamtenga huyo mtu kwa muda wa siku saba.

22. Kama ugonjwa huo utaenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; sehemu hiyo ina ugonjwa.

23. Lakini, kama ile sehemu haijaenea, basi, lile ni kovu la jipu tu. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi.

Walawi 13