Walawi 11:10-23 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Lakini chochote kinachoishi baharini au mitoni, ambacho hakina mapezi wala magamba, yaani viumbe vyote viendavyo majini na viumbe vingine vyote viishivyo majini ni najisi kwenu.

11. Viumbe hivyo vitakuwa daima najisi kwenu. Msile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao kwani ni najisi.

12. Chochote kinachoishi majini ambacho hakina mapezi na magamba ni najisi kwenu.

13. “Ndege wote wafuatao ni najisi kwenu; hivyo msile: Tai, furukombe, kipungu,

14. mwewe, aina zote za kozi,

15. aina zote za kunguru,

16. mbuni, kirukanjia, dudumizi, aina zote za kipanga,

17. bundi, mnandi, bundi kubwa,

18. mumbi, mwari, mderi,

19. korongo, aina zote za koikoi, hudihudi na popo.

20. “Wadudu wote wenye mabawa na waendao kwa miguu minne, hao ni najisi kwenu.

21. Lakini, baadhi ya wadudu wenye mabawa na wanakwenda kwa miguu minne ya kurukia ardhini mnaweza kula.

22. Hao ni: Kila aina ya nzige, kila aina ya senene, kila aina ya panzi na kila aina ya parare.

23. Lakini wadudu wengine wote wenye mabawa na miguu minne ni najisi kwenu.

Walawi 11