Walawi 1:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu alimwita Mose na kuongea naye katika hema la mkutano, akamwambia,

2. “Waambie Waisraeli kwamba kama mtu anapenda kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya mnyama, mnyama huyo atamchagua kutoka kundi lake la ng'ombe, kondoo au mbuzi.

3. “Kama sadaka anayotoa mtu ni ya kuteketezwa, atamchagua mnyama dume asiye na dosari kutoka kundi lake, atamtolea mbele ya mlango wa hema la mkutano ili apate fadhili ya Mwenyezi-Mungu;

4. ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mnyama wa sadaka ya kuteketezwa, ambayo itakubaliwa kwa ajili ya kumfanyia huyo mtu upatanisho.

5. Kisha, atamchinja huyo ng'ombe mbele ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani, wazawa wa Aroni, wataichukua damu na kuinyunyizia madhabahu mlangoni mwa hema la mkutano, pande zake zote.

6. Huyo mtu atamchuna huyo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa na kumkata vipandevipande.

7. Hao makuhani wazawa wa Aroni watazipanga kuni juu ya madhabahu na kuwasha moto.

8. Kisha makuhani hao watachukua vile vipande vya nyama, kichwa na mafuta, na kuviweka juu ya kuni juu ya madhabahu.

Walawi 1