4. Humo mlikuwa na madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kufukizia ubani, na sanduku la agano, ambalo lilikuwa limepakwa dhahabu pande zote, na ndani yake mlikuwa na chungu cha dhahabu kilichokuwa na mana, fimbo ya Aroni iliyokuwa imechanua majani, na vile vibao viwili vya mawe vilivyoandikwa agano.
5. Juu ya hilo sanduku kulikuwa na viumbe wenye mabawa, na mabawa yao yalitanda juu ya kiti cha rehema. Lakini sasa hatuwezi kusema kinaganaga juu ya mambo hayo.
6. Mipango hiyo ilitekelezwa, kisha ikawa desturi kwa makuhani kuingia kila siku katika hema ya nje kutoa huduma zao.
7. Lakini kuhani mkuu peke yake ndiye anayeingia katika lile hema la pili; naye hufanya hivyo mara moja tu kwa mwaka, na huwa amechukua damu ambayo anamtolea Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya makosa ya watu.
8. Kutokana na taratibu hizo Roho Mtakatifu anafundisha wazi kwamba wakati ile hema ya nje ingali ipo imesimama, njia ya kuingia Mahali Patakatifu sana haijafunguliwa.
9. Jambo hili ni mfano wa nyakati za sasa, ambapo zawadi na tambiko zinatolewa lakini haziwezi kuifanya dhamiri za wanaoabudu kuwa kamilifu,
10. kwani haya yote yanahusika na vyakula, vinywaji na taratibu mbalimbali za kutawadha. Yote hayo ni maagizo ya njenje tu; na nguvu yake hukoma wakati Mungu atakaporekebisha vitu vyote.
11. Lakini Kristo amekwisha fika, akiwa kuhani mkuu wa mambo yaliyo mema, ambayo sasa yamekwisha fika. Yeye anatoa huduma zake katika hema iliyo bora na kamilifu zaidi, isiyofanywa kwa mikono ya watu, yaani isiyo ya ulimwengu huu ulioumbwa.
12. Yeye aliingia Mahali Patakatifu mara moja tu, akiwa amechukua, sio damu ya mbuzi na ng'ombe, bali amechukua damu yake yeye mwenyewe, akatupatia ukombozi wa milele.
13. Watu waliokuwa najisi kidini waliweza kutakasika na kuwa safi waliponyunyiziwa damu ya mbuzi na ya ng'ombe pamoja na majivu ya ndama.
14. Lakini, kwa damu ya Kristo, mambo makuu zaidi hufanyika! Kwa nguvu ya Roho wa milele, Kristo alijitolea mwenyewe tambiko kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa dhamiri zetu kutokana na matendo yaletayo kifo, ili tupate kumtumikia Mungu aliye hai.
15. Hivyo yeye ni mpatanishi wa agano jipya ambamo wale walioitwa na Mungu wanaweza kupokea baraka za milele walizoahidiwa. Kifo chake huwakomboa watu kutoka yale makosa waliyofanya wakati wa lile agano la kale.