Waebrania 13:13-25 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake.

14. Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja.

15. Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu tambiko ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa kwa midomo inayoliungama jina lake.

16. Msisahau kutenda mema na kusaidiana, maana hizi ndizo tambiko zinazompendeza Mungu.

17. Watiini viongozi wenu na kushika amri zao; wao huchunga roho zenu usiku na mchana, na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha, la sivyo, watazifanya kwa huzuni, na hiyo haitakuwa na faida kwenu.

18. Mtuombee na sisi. Tuna hakika kwamba tunayo dhamiri safi, maana twataka kufanya lililo sawa daima.

19. Nawasihi sana mniombee ili Mungu anirudishe kwenu upesi iwezekanavyo.

20. Mungu amemfufua katika wafu Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha agano la milele.

21. Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze matakwa yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.

22. Basi, ndugu, nawasihi mpokee kwa utulivu ujumbe huu wa kuwatieni moyo. Hii ni barua fupi tu ambayo nimewaandikieni.

23. Napenda kuwajulisheni kwamba ndugu yetu Timotheo amekwisha funguliwa gerezani. Kama akifika hapa mapema, nitakuja naye nitakapokuja kwenu.

24. Wasalimuni viongozi wenu wote pamoja na watu wa Mungu! Ndugu wa Italia wanawasalimuni.

25. Tunawatakieni nyote neema ya Mungu.

Waebrania 13