Waebrania 13:11-19 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Kuhani mkuu wa Kiyahudi huleta damu ya wanyama katika Mahali Patakatifu na kuitoa tambiko kwa ajili ya dhambi; lakini nyama za hao wanyama huteketezwa nje ya kambi.

12. Ndiyo maana Yesu pia, kusudi apate kuwatakasa watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa na kufa nje ya mji.

13. Basi, tumwendee huko nje ya kambi tukajitwike laana yake.

14. Maana hapa duniani hatuna mji wa kudumu; lakini tunautafuta ule unaokuja.

15. Basi, kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu tambiko ya sifa daima, yaani sifa zinazotolewa kwa midomo inayoliungama jina lake.

16. Msisahau kutenda mema na kusaidiana, maana hizi ndizo tambiko zinazompendeza Mungu.

17. Watiini viongozi wenu na kushika amri zao; wao huchunga roho zenu usiku na mchana, na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu. Kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha, la sivyo, watazifanya kwa huzuni, na hiyo haitakuwa na faida kwenu.

18. Mtuombee na sisi. Tuna hakika kwamba tunayo dhamiri safi, maana twataka kufanya lililo sawa daima.

19. Nawasihi sana mniombee ili Mungu anirudishe kwenu upesi iwezekanavyo.

Waebrania 13