16. “Hili ndilo agano nitakalofanya nao, siku zijazo, asema Bwana:Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao,na kuziandika akilini mwao.”
17. Kisha akaongeza kusema:“Sitakumbuka tena dhambi zao,wala vitendo vyao vya uhalifu.”
18. Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa tambiko za kuondoa dhambi.
19. Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu.
20. Yeye ametufungulia njia mpya, njia ya uhai, kupitia lile pazia, yaani mwili wake mwenyewe.
21. Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu.
22. Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa kutokana na dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi.
23. Tuzingatie kabisa tumaini letu tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
24. Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema.