Ufunuo 14:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kisha, nikaona mlima Siyoni na Mwanakondoo amesimama juu yake; pamoja naye walikuwa watu 144,000 ambao juu ya paji za nyuso zao walikuwa wameandikwa jina la Mwanakondoo na jina la Baba yake.

2. Basi, nikasikia sauti kutoka mbinguni, sauti iliyokuwa kama ya maji mengi na kama ya ngurumo kubwa. Sauti niliyosikia ilikuwa kama sauti ya wachezaji muziki wakipiga vinubi vyao.

3. Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao watu 144,000 waliokombolewa duniani.

4. Watu hao ndio wale ambao hawakujichafua na wanawake, nao ni mabikira. Wao humfuata Mwanakondoo kokote aendako. Wamekombolewa kutoka miongoni mwa binadamu wengine, wakawa wa kwanza kutolewa kwa Mungu na kwa Mwanakondoo.

5. Hawakupata kamwe kuwa waongo; hawana hatia yoyote.

6. Kisha, nikamwona malaika mwingine anaruka juu angani akiwa na Habari Njema ya milele ya Mungu, aitangaze kwa watu waishio duniani, kwa mataifa yote, makabila yote na watu wa lugha zote na rangi zote.

7. Naye akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumtukuza! Maana saa imefika ya kutoa hukumu yake. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu na dunia, bahari na chemchemi za maji.”

Ufunuo 14