1. Kisha, nikaona mlima Siyoni na Mwanakondoo amesimama juu yake; pamoja naye walikuwa watu 144,000 ambao juu ya paji za nyuso zao walikuwa wameandikwa jina la Mwanakondoo na jina la Baba yake.
2. Basi, nikasikia sauti kutoka mbinguni, sauti iliyokuwa kama ya maji mengi na kama ya ngurumo kubwa. Sauti niliyosikia ilikuwa kama sauti ya wachezaji muziki wakipiga vinubi vyao.
3. Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao watu 144,000 waliokombolewa duniani.
4. Watu hao ndio wale ambao hawakujichafua na wanawake, nao ni mabikira. Wao humfuata Mwanakondoo kokote aendako. Wamekombolewa kutoka miongoni mwa binadamu wengine, wakawa wa kwanza kutolewa kwa Mungu na kwa Mwanakondoo.
5. Hawakupata kamwe kuwa waongo; hawana hatia yoyote.
6. Kisha, nikamwona malaika mwingine anaruka juu angani akiwa na Habari Njema ya milele ya Mungu, aitangaze kwa watu waishio duniani, kwa mataifa yote, makabila yote na watu wa lugha zote na rangi zote.
7. Naye akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumtukuza! Maana saa imefika ya kutoa hukumu yake. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu na dunia, bahari na chemchemi za maji.”
8. Malaika wa pili alimfuata huyo wa kwanza akisema, “Ameanguka! Naam, Babuloni mkuu ameanguka! Babuloni ambaye aliwapa mataifa yote wainywe divai yake – divai kali ya uzinzi wake!”
9. Na malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Yeyote anayemwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake juu ya paji la uso wake au juu ya mkono wake,
10. yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji. Mtu huyo atateseka ndani ya moto wa madini ya kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwanakondoo.
11. Moshi wa moto unaowatesa hupanda juu milele na milele. Watu hao waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa alama ya jina lake, hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana.”
12. Hivyo, ni lazima watu wa Mungu, yaani wale wanaotii amri za Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu.